LEO nakumbuka siku yangu ya kuzaliwa. Hili ni tukio ambalo katika mila za Kiafrika halikuwa na nafasi sana. Mara ya kwanza kwangu kufanya sherehe hii ilikuwa kidato cha sita pale Mkwawa. Mara nyingi sherehe hunikuta shuleni mbali na familia ya kwetu. Leo hii pia imenikuta hapa Amerika na vijana wamechachamaa sana kuwa lazima kuwepo na hafla. Inaonekana itakuwa hafla kubwa tu kwani rafiki zangu walikuwa wamesafiri kila mtu kivyake kwa ajili ya sherehe za Thanksgiving. Mimi nami nilikuwa Washington D.C na kisha Houston Texas. Nilirudi hapa siku mbili zilizopita. Kazi ni nyingi lakini kwa kuwa rafiki wanahitaji kunywa Juisi ya Maembe pamoja nami nimeona siwezi kuwakatalia. Lakini nakumbuka jambo moja ninapokuwa nakata mbuga ya siku za uhai wangu hapa duniani. Nashukuru kuwa Mwaka huu umeonesha dira halisi ya mimi kuwa kiumbe wa dunia hii. Ni jana tu nilipoanza majukumu ya kudurusu Utamaduni na Kiswahili kwa wanafunzi wangu wapendwa, wote mabinti wapatao watano hivi. Walifurahi sana jana na leo ninaadhimisha kuanza mwaka mpya. Naanza mwaka mpya huku Tanzania wiki ijayo ikifanya uchaguzi. Najua kuwa Kikwete atashinda lakini swali langu lipo katika Baraza lake la Mawaziri. Sidhani kama atafuata urafiki kugawa madaraka. Kama akifuata hivyo basi huyu jamaa tajiri mkubwa aitwaye Lowassa anayemfuatia Sumaye atakabidhiwa kiti hicho. Lakini nimekumbuka kuna mchezo humo ndani. Yawezekana nafasi hii kama uadilifu utafuatwa akapewa Mongella. Huyu mama anafaa na \ni wazi huu ni wakati wake kuhema na kucheka katika Tanzania baada ya kutamba sana katika duru za kimataifa. Mwaka huu murua sana maana kichwa changu kimepanuka sana katika masuala ya kisiasa. Mifumo ya mataifa haya makubwa nimejitahidi kuyasoma na kuyazingatia. KADRI SIKU ZIENDAVYO NDIVYO NINAVYOZIDI KUIVA. Siku mbili zilizopita kulikuwa na mafafali ya kuhitimu shahada ya kwanza pale Mlimani ambapo mimi nilipewa yangu. Haikuwa kama ya Mrema yangu nimeisotea kwa miaka minne na hiki ndicho kisa cha mimi kuanza jina langu na kuitwa Mwalimu Makene. Kuanza fani ya ualimu moja kwa moja na shahada ya Chuo Kikuu ni nadra sana katika Tanzania. Wachache hao ni mimi pia. Ni wazi kazi hii nitaifanyia kazi baadaye. Nitarudi kuongeza habari hii baadaye. |
Mwalimu Makene.. Nimekuwa na mawazo ya kutembelea blogu yako kwa juma zima ila nilikuwa mvivu kutafuta anuani yako,Ila leo nimefanya hivyo.
Mwaka mpya umeanza kwako, Hongera kwa kumaliza uliopita, na umalize salama miaka ijayo..
Natarajia utatumia mwaka huu kutupasha habari motomoto zaidi kwenye hiki kibaraza chako.