Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Monday, November 14, 2005
KUTENGWA HADI HAPA?
NILIAMKA mapema leo, na kuanza kupanga kila nilichonacho ili kuiwakilisha Afrika. Tangu jana nilishafanya azimio la kuchukua kazi ya kulitangaza Bara hili na sio kuitangaza Tanzania pekee. Sababu kuu iliyochagiza hili ni mgomo unaotokana na kutotolewa hadi sasa nakala za maandishi yanayobainisha uhalali wa uwepo wa Tanzania. Aibu hii, yaani maandishi kama hayo hadi tufikishane mahakamani. Mfalme Mkapa analijua hili...ukimya wa nini au naye hana maandishi hayo! Kesi hiyo inapaswa kufunguliwa pia na wakazi wa Tanganyika maana nao tunahitaji maandishi haya!

Nimefika katyika ukumbi tunaoweka mabango yetu na kukuta ni wakati wa maandalizi. Nikaweka Bango langu jirani na hawa wajinga kutoka Ufaransa. Baada ya kuliweka ama niseme kuliegesha nikatoka na kukimbilia takwimu fulani. Kurudi, nasikia mmoja wa wajinga hao ananiomba kuwa nihamishe bango langu ili wakae karibu na wawakilishi wa Ujerumani.

Nikawajibu kwa Kiingereza cha dharau, "I dont care even if my chance is going to be ommited," nikatazama pembeni na kisha nikahamisha makazi yangu mbali na mabango ya washenzi hawa! Huko nikaweka sehemu wanapoweka taarifa za Chuo hiki na kisha nikatokomea darasani kusikiliza mhadhara wa sera za mambo ya nje za Marekani.

Nikiwa huko kuja huyu jamaa yangu toka Saudi Arabia akanipigia simu. Nikaizima maana sikutaka usumbufu. Ninapofika tena naambiwa waliweka Bango langu sehemu jirani na Saudia. Nawatazama kwa jicho chafu kisha naanza kutoa darasa. Kuna jamaa anakuja hapa ninamkatia taarifa za Afrika na kisha kumwagia mfumo hasi wa siasa zetu. Anacheka na kisha anaongezea naye juu ya maisha ya serikali ya Bush. Nacheka nami.

Mchana unazidi kukatika na jioni hii ninapoandika hapa natakiwa kuwakilisha vazi la Tanzania. Hatuna vazi sisi na wala sishabikii tuwe nalo. Najua tukiwa nalo litakuwa ghali na wataweza kulivaa hawa wafalme na watoto wao pekee. Inawezekana kabisa likatumika kama chanzo cha Rushwa ya Takrima. Na inawezekana kulipata kukatakiwa kibali maalum kama ilivyo kwa kile Kitambaa cha Taifa.

Nimepiga hii sarawili kama kengere ya Bomani. Namshukuru sana Matukio Chuma kwa kuniwezesha na hiki kiwalo. Nitatinga na shati lake baadaye na kupita stejini kama mtangazaji mavazi. Kuna jamaa wamekuwa wakitoa sifa kwangu kuwa namudu kazi hii, sijui kama atapatikana mtu wa kuninunua nifanye kazi hii maana nasikia nayo inalipa!

Nikitoka hapo nitakimbia hapa Maktaba kuweka taarifa zangu murua maana kesho nina kazi ya kumwaga sera. Hapa sitatoa takrima ili nisikilizwe. Nitazungumzia Afrika, sitaficha pale niulizwapo. Nitawapasha na kuchomekea suala la Iraki japo kidogo. Kisha nitawakumbusha kuwa Kampeni za huku kwao zimeanza mapema mno na inawezekana John Kerry akawa na kazi ngumu lakini ni wazi kuwa Mama Klintoni sidhani kama ana lake. Unajua kwa nini? Kama alishindwa kumlinda mumewe asirubuniwe na Monica Lewinski atawezaje leo kuliongoza taifa kama Marekani?

Kazi ipo sasa natakiwa kukimbia kutinga kiwalo changu najua kidogo nitafanana na namna Ndesanjo anavyoshamiri katika Blogu lake.
 
© boniphace Tarehe 11/14/2005 03:26:00 PM | Permalink |


Comments: 2


  • Tarehe 11/14/2005 5:46 PM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

    Hapana Makene tunaweza tu tukawa na vazi la Tanzania, kunradhi nilitaka kutamka Tanganyika ila ulimi umeteleza kidogo tu. Au tunaweza tukawa na mavazi ya taifa ya aina mbili ama tatu kutokana na tabaka halisi la mwananchi husika. Wazo langu tuanzishe vazi la magunia kwa tabaka la akina pangu pakavu tia mchuzi. Nafikiri hatutatakiwa kuwa na passport kupata magunia kama yale ya iliyokuwa nesho milingi. Au unasemaje.

     
  • Tarehe 11/14/2005 6:43 PM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Kaka acha kututukana hivyo, unajua niliwahi kulalia hayo magunia nyakati zile magodoro wakitumia wafalme wetu? Ulikuwa ukikutwa na godoro unaitwa mhujumu uchumi, linachukuliwa na hujui linapopotelea?

    Kaka yale magunia yanavyowasha na nyumba zetu kuna kipindi zinakabiliwa na chawa sasa hapo panakuwa patamu yaani bora hata kujikuna kwa mgonjwa wa Ukimwi kuliko chawa watakaotokana na magunia hayo unayotaka tuyafanye vazi la walala hoi wa danganyika

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved