Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, November 01, 2005
KARUME KATANGAZWA, VIPOFU KUONA MWANGA!
TAARIFA nilizozipata asubuhi hii ni pamoja na kutangazwa kwa Karume kama mshindi wa Urais wa Zanzibar. Matokeo hayo yametangazwa huku mgombea wa CUF, Seif Shariff Hamad akiwa kakataa matokeo kabla hata hayajatangazwa kufuatia kile alichokisema kukithiri kwa hujuma na ghiliba za kupika matokeo kama ilivyofanyika katika chaguzi zilizopita.

Kuna utitiri wa watu walioombea Tanzania isifikie matokeo haya matharani katika mazingira yanayoonyesha kuwepo giza la kupatikana ushindi. Yale maroli yaliyopakia wapiga kura, mabomu ya polisi kwenye vituo, utata wa majina kwa wapiga kura na kundi kubwa la wapiga kura kukosa kupiga kura ni sababu chache tu za kuonyesha namna Tanzania inavyochezea ulimwengu na kuamini ina nguvu hata za kuhimili mataifa makubwa kiuchumi!

Mazingira ya tume ya uchaguzi kuwa pofu na kuonyesha upendeleo yalianza wakati wa kugawa majimbo ya uchaguzi, huku majimbo ya Pemba yakipunguzwa kimakusudi na kuongezwa yale ya Unguja. Kama hiyo haitoshi usiri na utata wa daftari la wapiga kura ambapo awali iliripotiwa kutumika kampuni ya Waymark toka Afrika Kusini kulihakiki kitaalamu lakini ikapigwa ngwara na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hitimisho likawa matumizi ya wataalamu wa ndani waliopewa deal hilo bila kubaini zana walizokuwa wakitumia ukitambua kuwa Tanzania iko nyuma katika teknolojia.

Haya maombi ya wengi ni kuhusu kutotokea machafuko katika Tanzania maana si utani nchi inaonekana kuelekea huko maana uchovu na hasira sasa zitakuwa zimepanda sana kwa wakazi wa Pemba na mashabiki wa CUF.

Mfalme Mkapa anaondoka Januari na huo utakuwa muda mzuri wa kulitupa taifa katika machafuko. Kuna hatari aina ya siasa za Tanzania kubadilika kufuatia kuwepo giza la usiri na kutokuwepo mazingira ya dhati katika kufikia hatma ya kukubali kushindwa na hasa kwa SERIKALI ZINAZOONGOZA NCHI HIYO.
 
© boniphace Tarehe 11/01/2005 06:52:00 AM | Permalink |


Comments: 3


 • Tarehe 11/02/2005 5:35 AM, Mtoa Maoni: Anonymous Anonymous

  Mzozo, mzozo, mzozo huo...

   
 • Tarehe 11/04/2005 7:54 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

  Mwenye kuunda tume ni yeye, anayemiliki jeshi na silaha ni yeye, mwenye kuhesabu kura yeye, anayetangaza matokeo yeye...Karume huyo. Ndio wanaita demokrasia ya chama twawala!

   
 • Tarehe 11/04/2005 10:36 AM, Mtoa Maoni: Blogger Boniphace Makene

  Hayo ndiyo matunda ya kusubiria haki mezani. Afrika ni haki yetu tutajwe kuwa tunapenda ukatiri na mauaji. Kama vyombo vya dola vina kazi ya kutunza miliki za wafalme fulani ambao ndio hao hao wanaowanyima masiaha bora unadhani tutafika lini Ndesanjo.

  Kuna kazi nasema kuna kazi. Hapana hapana nasema hapana, haivumiliki haivumiliki, sitaki sitaki sitaki kuona, nalishwa nini hiki, sumu geuzwa asali, sili nasema sili na sizibi mdomo!

  Hasira zimenifanya kuanza kutunga shairi bila kutarajia. Nakumbuka mashairi ni liwazo la wenye akili razini, fundisho la wenye dhiki na faraja kwa wenye heri. Baadaye Ndesanjo nitapitia kwenye ukumbi wako pia kukusalimia.

   
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved