Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, November 26, 2005
HAPANA VITA, BORA KUFIA HAPA WHITE HOUSE
Picha niliyoibandika hapa chini haikuwa na maana ya kuonyesha sura yangu. Ililenga huyo mama aliyeshika mabango nje ya ikulu sasa akitimiza miaka 24 kwa kazi hiyo ya kukaa saa 24 kupinga vita na matumizi ya Nyuklia ulimwenguni. Kumbuka eneo la Washington D.C lilivyo na baridi kali, haya ni majitoleo yanayotakiwa kupewa heshima. Kwa miaka yote hiyo amekuwa hapo nje ya Ikulu ya Mrekani akionyesha hasira zake na hii inatoa picha walau namna wenzetu wanavyoweza kuthamini uhuru wa mawazo ya wenzao kwa kuyatazama na kuyasikiliza hata kama hawayafanyii kazi. Katika Tanzania hata kukenua kinywa chako kutaka kusema ni kosa litakaloambatana na wewe kupigwa bomu na upupu uliochanganywa katika maji ya askali waitwao FFU.

Wiki iliyopita hapo Tannzania Kamanda wa Serikali katika Jeshi la Polisi aliwatishia Madktari waliokuwa katika mgomo kuwa kama wanataka kumuona Ziraili basi washinikize kuandamana kwenda kuwasumbua katika usingizi wafalme wa Tanzania wanaokaa ikulu ya Mgogoni. Kwa picha ya kawaida naomba ufahame wewe ambaye hukuwahi kufika ikulu ya Tanzania. Imezungushiwa ukuta mrefu sijui.. maskini kama mimi nasikia tu kuwa kodi zangu zatumika kuikarabati na wanaotanua humo sijui wana maana gani kujifungia ndani kiasi hicho? Wanamuongoza nani na lini walala hoi walipata fursa ya kukaribia ukuta huo kama hawataishia Ukonga kukaribisha kulawitiwa na kunyea kwenye debe!

Miaka ya huko nyuma raia wa Marekani waliweza kuingia hadi White house bila vizuizi, siku hizi kumewekwa uzio wa vyuma vya wazi. Nyuma yake kuna uwanja unaozungumzwa katika makala hii. Hapa ni sehemu ya kutolea dukuduku la kila raia. Maandamano mengi huishia hapa na ni jirani kabisa na ikulu kubwa duniani. Kwa nini Tanzania madaktari wametishiwa kupigwa mabomu kwenda ikulu yao wanayoilipia kodi kuikarabati?

Uhuru wa kusema hata yauchomayo moyo umefupishwa sana katika Tanzania. Kuna tabaka linalodhani kuwa ndilo linaloweza kukalia fikra za watu. Hawa Wafalme wakiongozwa siku hizi na huyu Mfalme Mkapa wanadhani wao ni bora zaidi kuliko wadanganyika wengine. Kimsingi wamelewa madaraka, wanafuta na kuzuia kila linalotokea, wanatumia majeshi kujilinda kama wafanyavyo wafalme katika miliki zao. Wameigeuza nchi na hata kuifananisha na Iraki iliyoko katika vita sasa.

Bibi huyo hapo amekaa hapo akipinga vita hivyo kwa miaka 24, kumbuka ni serikali ngapi zimepita tangu huyo bibi aanze kukaa hapo jirani na ikulu. Ingekuwa Tanzania sijui maana kama wapinzani waweza kulindwa na kufungiwa vijijini huko Pemba.
 
© boniphace Tarehe 11/26/2005 11:40:00 AM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved