Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Thursday, October 20, 2005
SALAMU KWA WANA GOFACHOA
Natanguliza kuwasalimu bila shaka ni kitambo nimekuwa mbali nanyi. Nafurahi kupata taarifa za maendeleo kupitia vyanzo visivyo rasmi. Bila shaka huu ni wakati wa kukamilisha mazingira magumu ya kuiandaa GOFACHOA kuanza kupaa kiuchumi. Huu ni mkakati unatakiwa kufanywa kwa kuangalia kaida za wanachama na mazingira ya aina ya uchumi wanaoamini unaweza kuwapaisha wao na jamii wanayoitumikia.

Nitumie fursa hii, kuomba nami kupata taarifa za msingi za kimaendeleo za GOFACHOA huku nikitoa hamasa ya kutimiza majukumu ya sasa maana wakati unakimbia kwelikweli, narudia tena, wakati unakimbia kwelikweli.

Majukumu katika asasi hizi zisizo za kiserikali yanahitaji mabadiliko ili asasi kama hizi zilenge majukumu nje ya wanachama na kuwafikia wananchi. Zinapaswa kuwa mhimili wa kuwasaidia wanyonge maana zinawafikia kabisa kuliko kushiriki vita vya kuwanyonya wanyonge.

Mataifa makubwa hutumia asasi hizi kutoa msukumo wa aina gani serikali ziwaongoze wananchi na pia mgawanyo wa bajeti za serikali hizi. NGO zina mchango mkubwa na hili halikuja kama zawadi, ni zao la majitoleo na shutuma nyingi za wale waliokubali kupambania mazingira hayo. Kwa kiasi kikubwa walijitahidi kutofautisha mazingira ya kuziendesha ili yasirandane na madaraka ya kisiasa. Siasa imekuwa na mihimili mingi inayoipatia fursa ya kuwa katika majaribio karibu kila siku.

NGO zaweza kushika suala moja zikalisimamia kupia raslimali ndogo zinazozunguka eneo la NGO husika. Mtindo wa NGO kuendeshwa kupitia wahisani na wafadhili ni moja ya matukio ya unyonyaji yanayoiandama sasa Tanzania. Kauli hii inaweza kubaki kuwa mtazamo wangu lakini kumbukeni kuwa hakuna aliye na upendo wa kuondoa umaskini wa watanzania zaidi ya wenyewe kwanza.

Ni wazi tuna malengo mazuri na wengi wetu sasa tumekua na ujuzi wetu unaongezeka. Siku si nyingi tutakuwa na uchaguzi mwingine na hapo tutapima tulipotoka na tulipofika na majukumu yetu ni yapi huko tuendako.

Wajibu wetu utabaki palepale na kushindwa kutabakia zawadi ya kutojitutumua kufika mbele. Mbinu moja na nyingine zapaswa kuhusishwa ili kufika mbele na hakuna mkono unaoweza kujenga nyumba bila kushirikisha viungo vingine vya mwili. Kama tunafanikiwa basi lazima mafanikio hayo yahusiane na umma maana umma ndio unaoyataja mafanikio na kuyakubali. Kama tunashindwa inawezekana ni kutokana na kushindwa kuupa umma nafasi ili tufikie mafanikio. Huu ndio mhimili wa kuendesha NGO ili zifikie malengo.

Naambatanisha salamu za dhati kwenu wana GOFACHOA.
 
© boniphace Tarehe 10/20/2005 04:54:00 PM | Permalink |


Comments: 0


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved