Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Tuesday, October 11, 2005
NAJIBIA HAPA

Nimechoka kuulizwa sawali hili na sasa najibia kupitia Blog yangu. Asiyesoma hapa tafadhali nimechoka kuulizwa! Nipo Marekani kudurusu Kiswahili naamini kila Mtanzania anafahamu kuwa Mimi Mwalimu na masomo yangu ni Kiswahili na Kizungu. Hayo ndiyo niliyosomea hapo Mlimani na kupata shahada yangu ya kwanza.

Kwa sasa nipo hapa Texas kwa kazi ya kuanzisha somo hili kuwa la kudumu hapa. Makujumu haya mazito sana lakini nashukuru Marekani kuniamini kunipa mimi kazi ya kuanzisha Kiswahili katika Jimbo hili la George Bush. Huyu Bush alikuwa Gavana wa Jimbo hili na hii ni moja ya sababu ya mimi kufurahi kuwepo maskani kwake hapa.

Kazi yake ya awali ni "Mfanya Biashara wa Mafuta" sitaki swali maana hii nimesoma katika Kitabu cha Siasa za Marekani na Texas na sihusishi kabisa suala hili na vita ya Irak. Hapa Vyuo vikuu vina miradi ya visima vya mafuta lakini Bongo kazi ya akina Luhanga ni kuuza Ardhi ili kujenga Makasino wakati vijana hawana pa kusomea na kulala.

Nitakuwa hapa usiniulize hadi lini maana hufanyi kazi Uhamiaji. Na hata kama unafanya kazi huko hapa nipo Marekani na sio Tanzania. Siku chache zijazo nitakupa michapo ya Ranchi ya Bush iliyopo katika mji mkuu wa Texas Austin. Ni katika Ranchi hii alipokuwa akiponda raha mzee Bush wakati raia wakiswagwa na Katrina. Sijui ni mvinyo gani alikuwa akinywa lakini amekuwa akitamka mara kwa mara kuwa ameokoka lakini anaweza kuchanganya juisi na damu za askari wa Marekani na zile za raia maskini kule Irak na Afghanistan.

Naweza kusema haya huku maana uhuru wa matamshi umewekwa katika Katiba tangu miaka ya 1770s na kikawekwa kifungu kuwa Congress haiwezi kubadili haki hii. Kwa hali hiyo yaani napumua kwa mtaji wangu tu. Ee Mungu nisaidie.
 
© boniphace Tarehe 10/11/2005 10:17:00 AM | Permalink |
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved