Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Friday, October 28, 2005
KILA LA HERI ZANZIBAR, LAKINI MSHINDI APEWE CHAKE!!
NIMECHOKA kusikia kelele hizi, miaka sasa yakatiza na kufikia kumi na ushee! Kelele hizi zaniumiza na kunikera sasa. Watoto hawa wamegeuka tishio katika KASRI na mwanazuo nashindwa kupanga aya za maandishi ya hekima sasa!

Mwaka 1995, walikuja na kulia machozi makavu na kuna chombo kikatangaza kuwa walipewa kitumbua na wavuvi wa bahari ya Hindi lakini akatokea PAPA akakikwapua kwa nguvu akakitupa baharini! Nasikia kabla kitumbua hakijafika baharini PAPA huyo akaamua kukila kabisa!

Watoto hawa wakalia na machozi yao hayakusikilizwa hadi mwaka 2000, ambapo pia wavuvi wakaamua tena kuwapa kitumbua kilichobaki. Hizi hadithi nimekuwa nikizisikia sana na nimeona leo niziweke hapa. Walipotaka kufunua kinywa wakaibuka wajanja tena na kukitia mchanga kitumbua huku watoto hao wakitazama!

Wameitwa watoto kwa sababu eti hawana uzoefu, na mfumo wa utawala hawaujui kwa kuwa walizaliwa mwaka 1992. Kuna jamaa mmoja alitangaza wazi kuwa hawafai kupewa Mke kwa kuwa watashindwa kumtunza!

Sasa Jumapili hii wanacheza tena mchezo wa kutafuta kitumbua chao ambacho inasemekana kimekuwa kikichukuliwa mikononi pasipo mazingira safi! Kama kuna ukweli huu kuna haja sasa simanzi za Januari 27, 2001 kukumbukwa na kukubalika kitumbua kupewa mshindi.

Sitaji wavamizi na wakimbizi hapa, Kasri langu si hekalu kubwa na siwezi wakilimu wote. Hata hivyo nimekumbuka kuwa hapa chakula chetu fikra na ni wachache watakaokubali kukaa katika kasri hili wakati machafuko yakitokea tena Zanzibar.

Yale mliyokuwa mkiyaita Mapinduzi mengine kama alivyonukuliwa kijana aliyezaliwa katika mauaji ya Zanzibar ya mwaka 1964, namuomba asithubutu kutishia maana damu za Watanzania si mali yake na familia yake. Anaweza kupata madaraka lakini si kuchangia kukwapua madaraka kwa nguvu!

Tunataka haki hapo Zanzibar maana huko Bara hakuna uchaguzi nashangaa kwa nini wameahilisha wakati Rais anafahamika. Wajinga hawa wanampenda sana Mfalme Mkapa na wameona wamuongezee muda yeye na mkewe kuendelea kuchuma na kuweka mahesabu sawa. Haya twatazama huku fikra zikipamba moto
 
© boniphace Tarehe 10/28/2005 11:26:00 AM | Permalink |


Comments: 1


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved