Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Sunday, October 16, 2005
GUMZO KUBWA,SASA NAONGEZA!!!
MSIBA wa Hayati Mutie kama alivyoitwa na Nipashe unazidi kuzua gumzo. Ningetamani kaka yangu Benjamin afariki sasa, alikosa matibabu wakati akiwa mfanyakazi wa serikali, Mwalimu aliyeacha wanafunzi baada ya kutoa huduma kwa miezi sita tu. Hakukuwa na ukaribu wa kumtibu mpendwa wangu huyu. Alipofariki hatukupewa JET au herikopta ya serikali ili kumfikisha nyumbani kwake kisiwani Irungwa kwa amani! Alilala akipulizwa na mawimbi ya maji. Nitaandika zaidi kisa hiki. Sasa nachukua ugali kula hapa kwa ndugu yangu Said Mkomola, baada ya ugali huu nitakuwa njiani kwa basi muda wa saa kama kumi hivi kurudi Edinburg. Nikifika huko nitaongeza kisa hiki ambacho sasa ni mjadala hasa.

NILIFIKA jana jioni Mc Allen na baada ya hapo nilichukua Taxi kuja nyumbani Edinburg. Ulikuwa usiku na nilipata muda wa kulala kidogo. Sifahamu kama familia yangu iliwahi kupata hata mazingira ya kutazamwa afya zao maana kama hili lingelikuwa linafanyika kwa wafanyakazi wa serikali Tanzania huenda mwalimu Benjamin asingelifariki mapema mno.

Natambua kuwa, serikali haina mikakati ya kuwapa fursa wananchi kujua na kutunza afya zao lakini ni hiyo hiyo serikali inayowalipa mishahara kidogo. Mishahara hiyo inawafanya kushindwa kulipa gharama za huduma zao za afya na huwezi kuamini wengi wa wafanyakazi ndio wanaojipanga kupata huduma za MEWATA baada ya kungoja kuchangiwa na wasamalia.

Hii ni aibu na inatia simanzi, kama wafanyakazi wa serikali hawawezi kupata huduma za msingi kama afya itakuwaje kwa wananchi maskini vijijini wasio na kipato na hasa hawa wanaotegemea malipo ya mazao ya biashara: mazao yenyewe ni yale yanayopatikana baada ya Mungu kuona huruma na kumwaga mvua yake?

Hadi lini Tanzania itakuwa hivi na ubaguzi huu kutokana na mali utaishia wapi! Siamini kama nikifa hapa msiba wangu utakuwa mkubwa kutokana na jina la Baba yangu. Si kweli na haitakuwa hivyo, nitazikwa na makabwela wenzangu na huenda wanasiasa watajileta ili kupata muda wa kujitangaza kupitia televisheni na magazeti.

Hali hii itatokana na kuwa sasa nafahamika kama mmoja wa wanamikakati ya kuwazungumzia wapiga kura. Nahisi usingizi na pia namtazama Benjamin hapa namna alivyokuwa akibabuliwa na moto pale Ocean Road! Hawana zana za kutosha kama ilivyo hapa Marekani na sijui wanataka nani apeleke zana hizo huko?

Kazi ya kukiamsha kizazi cha Tanzania na kukipa picha kuwa hakuna lisilowezekana inatakiwa kufanyika sasa. Hakuna kungoja maana hata huku kulikuwa kama Tanzania lakini jamii hazikulala zilikubali mabadiliko. Hakuna haja ya kukalia maneno na tabia hizi za kutumia kodi ndogo za walalahoi kuwanufaisha au kuwapendezesha ambao tayari wanakula pepo hapa duniani! Amkeni, sasa, chukueni njia hii, piteni na ketini nami katika Kasri hili, mwisho tutapata weledi wa kufuta upofu wetu.
 
© boniphace Tarehe 10/16/2005 10:57:00 AM | Permalink |


Comments: 2


   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved