Kasri, jumba la weledi waweza keti hapa na kupata ukitakacho. Chakula cha wakazi wa Kasri ni fikra na chakula hiki kimewapa thawabu wananchi wa nchi hii hali inayowafanya kutoziba midomo yao kila waonapo damu ya wanaonyanyaswa ikidondoka katika bahari ya dhiki, maangamizi na unyonyaji. Waweza nawe keti hapa na kula fikra hizi.
Saturday, November 12, 2005
NINAPOKOSA KAZI, KISA MGAWO WA MAJI NA UMEME DAR
NILIAMKA mapema jana nikaanza kutafuta nguo za kuvaa katika maboksi niliyoyapanga katika chumba hiki cha rafiki yangu. Jamaa huyu amekuwa akinihifadhi hapa siku nyingi, ee Mola mbariki huyu ndugu apate, aendelee kusaidia wajawako!

Ni wiki tatu tangu maji yakose hapa na hakuna namna ya kuyapata. Kila nikijitahidi kutembea zaidi kutafuta maji, ndipo ninapokabiliwa na jasho kali na uvundo unaotokana na jasho la jua la Dar. Sijaoga nina siku huku nikikabiliwa na haya, mosi sina kipato cha kununulia sabuni, mafuta mazuri na hata pafyumu nilishazisahau tangu nimalize Chuo Kikuu Mlimani.

Kukaa kwangu Dar kumembatana na kupinga mizinga washkaji kadhaa na sasa inafikia kila nikionana na mmoja wao ananikacha. Ninapokaa naogopa kuomba pesa ya kununulia maji ili nifue maana jamaa huyu ananipa usiongizi na pia chakula hivyo kumuongezea matumizi ni sawa na kashfa, kashfa inayoweza sababisha nifukuzwe na sijui akifanya hivyo nitakaa wapi!

Hapa mtaani umeme umetoweka sasa una wiki tatu na Jumatatu hii inayofika sasa nitakuwa nikienda kujaribu bahati ya kupata kazi. Nimeitwa kwenye usaili katika Kampuni moja ya Ulinzi, kazi isiyofanana na elimu yangu lakini nifanyeje!

Kumepambazuka sasa na shati langu licha ya kuwa na kauvundo hivi lakini halikupigwa pasi. Hakukuwa na umeme na pia sikupata maji hata ya kujiogesha mimi. Nashika njia ikiwa bado mapema maana natembea kwa mguu kutoka hapa Ubungo River Side hadi Faya.

Nafurahi nimefika mapema na hakuna wengi walioniona, nilijilawa na hapa ofisi haijafunguliwa. Natazama mlango wa ofisi hii na ghafla mama mmoja ananiuliza, "Wewe kijana unatafuta nini hapa mapema hii?" Nashindwa kumjibu namwambia tu nipo namsubiri mgeni wangu!

Uongo mbaya, na hili ni kosa la kwanza, sikufahamu kuwa mama huyu naye atakuwa kwenye usaili wangu. Ninapoingia katika usaili anaanza, "Wewe kijana si nilikukuta hapo nje nikakuuliza na hukunijibu? Vijana kama ninyi wahuni hamna nafasi hapa kwanza tazama nguo ulizovaa kweli wewe waweza kufanya kazi hii? Elimu yako ni ipi ebu toa vyeti?

Napata liwazo anaponiuliza juu ya vyeti, namtolea cheti changu cha BA Sociology cha Mlimani anakitazama na kisha sura inaonyesha kuwa tofauti nami. Nimechoka sifanani na tai niliyofunga katika picha hiyo. Ananitazama huku akionyesha kukerwa na harufu mbaya niliyojaza ukumbini hapo! Ananiambia naweza kwenda na kwamba nitapewa majibu baadaye!

Ninapotoka ukumbini hapo nabaini kuwa siwezi kupata kazi hiyo, napiga konde na kuanza safari yangu ya mguu huku nikiwa sijatia chochote kinywani. Maji ni kero sasa Dar es Salaam. Kingine ni huu Umeme ulioletewa wataalamu wanaolipwa mabilioni huku mimi na wenzangu tukikosa kazi. Eti wanaitwa Net Group Problem kampuni la uasimamizi toka Afrika Kusini.

Kampuni hili na lile lingine analolisimamia Mfalme Lowassa leo limechangia kuniweka katika mazingira haya ya kukosa hata haka kakazi nilikokuwa na kila sababu ya kukapata. Kuna wakazi kibao sasa wanaharisha na kipindupindi kinapiga chabo pale Mabibo Hosteli. Wanafunzi kibao wa Mlimani wanaokaa kule Changanyikeni nasikia wanatoroka nyumba zao na kujibanza vichakani kujisaidia. Hakuna maji na joto la Bongo linaonyesha wazi makucha yake.

Huko Kijijini Mabuimerafuru Mama yangu analalamika miguu inamuuma. Ananiomba mwanaye nitume walau kijibaisikeli ili waweze kukitumia kuchotea maji ziwani, mwendo wa masaa matatu kwa miguu. Miaka 40 tangu uhuru wanahangaika na adha hii huku wakiyatazama maji ya ziwa Viktoria yakipangiwa mpango sasa wa kusafirishwa Dodoma ili kuwapa ahueni wakubwa akina mzee Malecera na wenzake wakati wa vikao vyao vya kunyonya nchi.

Sina kazi, kila kona ni adha, maji, umeme, chakula, kodi za nyumba. Tena huyu mwenye nyumba mshenzi sana, jana kaja kudai kodi za umeme wakati sijawahi kuona cheche zake sasa nina wiki tatu. Nitampiga huyu nipelekwe Ukonga walau nikale bure...naogopa kupigwa mtungo huko maana hayo mambo ya Mombasa mimi sijawahi kuyafanya!

Tabu hii, hadi lini naona wakubwa vitambi vinatoka na maisha yao ya unono tu huku wakibadili mabenzi. Nifanyeje naanza njia nyingine.
 
© boniphace Tarehe 11/12/2005 12:32:00 PM | Permalink |


Comments: 6


  • Tarehe 11/13/2005 1:30 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

    Bwana. Hii makala imenifanya nijisikie hoi sana. Nashindwa nianze kusema nini. Net Group Confusion wanaita siku hizi. Kazi yao ni kukusanya pesa hata kama umeme hakuna. Wakishafika lengo la kukusanya wanalipana "Bonus". kazi yao si kuhakikisha kuwepo umeme. Mkataba wao ni kukusanya. Basi. Nimechoka. Siwezi kuandika tena. Lakini la kwenda Ukonga kula bure nalo limeniacha hoi. Madhara sasa ya kula bure!!

     
  • Tarehe 11/13/2005 8:32 AM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Dada Idya, kuna wakati fikra zinakwama kusoma mbele, hawa jamaa waliletwa kwa mbwembwe sana na mfalme Mkapa, hakuna walichofanya na miaka inayoyoma tu.

    Mwisho wa siku ni kuavamia ili tugawane hizo fedha wanazotukomba sisi wakesha hoi

     
  • Tarehe 11/14/2005 1:54 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

    Makene. Rekebisho kidogo. Mimi siyo dada. Ni Mkaka. Ni kweli nakumbuka mbwembwe na matusi ya Mfalme kwa watu hawa. nakumbuka jinsi alivyosema kwamba sisi tulishindwa kuiendesha TANESCO. Japo alisema kwamba TANESCO ilikuwa ikiendeshwa kwa hasara toka 1997 mpaka alivyoamua kuwaleta hao jamaa mwaka 2001 au 2002? sikumbuki vizuri. Alichosahau kutuambia ni kwa nini angoje miaka hiyo yote bila kubadilisha uongozi wa shirika lililokuwa likileta hasara kubwa.

     
  • Tarehe 11/14/2005 6:00 AM, Mtoa Maoni: Blogger Ndesanjo Macha

    Haya ndio mambo yanayonifanya niseme kuwa tunapaswa kutumia haki yetu ya kikatiba na kibinadamu kukataa upuuzi kama huu wa shirika la umeme. Wezi na waongo watupu. Swali la Nkya nami nalirudia, kwanini m-twawala mkuu asubiri miaka yote hiyo kama shirika lilikuwa linaendeshwa kwa hasara?

     
  • Tarehe 11/14/2005 6:37 AM, Mtoa Maoni: Blogger boniphace

    Ndesanjo kuna kijana wangu huko Bongo kanitumia mpya. Hii inatokana na angaika jana ya kushindwa kuwa online nami kutokana na kukosekana umeme. Anasema na hapa sijafanyia uchunguzi kwanza kuwa, hiyo NET pROBLEM INA MKONO WA ANNA MKAPA. Nadhani Idya yuko katika eneo jema la kuweza kutupa hii huku nami nikijitahidi kuchimbua maana huu ni wakati wa kuweka sawa dhambi za familia ya MFALME MKAPA dhidi ya matumizi ya mali za Wadanganyika

     
  • Tarehe 11/14/2005 8:52 AM, Mtoa Maoni: Blogger Indya Nkya

    Makubwa haya makene. Ukweli utadhihiri karibuni. Huyo mama ana mikono kila mahali basi. Yalisemwa mengi wakati hao Net Group Confusion walipokuja. Moja ya lililosemwa ni kwamba shemejiye na mfalme ndiye ana mkono huko.

     
   
 
Copyright 2006 © BONIPHACE MAKENE. All Rights Reserved